Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Mbeya, Mhashamu Godfrey Jackson Mwasekaga, amewataka wanakwaya Katoliki nchini Tanzania kupendana, kutakiana mema na kuvumiliana katika utume wao. Wito huu aliutoa wakati wa kilele cha Kongamano la kwanza la Kit
Wito huo ulitolewa na Mhashamu Godfrey Jackson Mwasekaga, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Mbeya wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Kilele cha Kongamano la kwanza la Utume wa Kwaya Katoliki Tanzania (UKWAKATA) Kitaifa Septemba 14, 2025 Dominika ya Kutukuka kwa Msalaba Mtakatifu katika Ukumbi wa Chimwaga ulioko ndani ya Viunga ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Jimbo Kuu Katoliki Dodoma.
Askofu Mwasekaga alisema utume wa kwaya katika Kanisa ni chombo cha kueneza upendo, hivyo kama wanautume huo wanatakiwa kupendana katika maisha kwa kuiga upendo wa dhati aliounesha Yesu Kristo msalabani alipotufia sisi wadhambi.
Pia aliwataka Wanakwaya na Waamini wote kutokukata tamaa wanapokutana na vitendo vya dhihaka na changamoto mbalimbali bali wavae hali ya uvumilivu kwa sababu kujua namna ya kusubiri katika maisha huleta mafanikio makubwa na hapo ndipo kila mmoja anaweza kuvuna matunda ya utume wake ndani ya Kanisa.
“Yesu hakujibu dhihaka yao, alivumilia, alikuwa na subira, kujua namna ya kusubiri katika maisha ni siri kubwa ya mafanikio, kwani subira huvuta heri, mvumilivu hula mbivu. Katika maisha tusikate tamaa, kuna watu watapita kutuletea kejeli mbalimbali, kuamsha hasira yetu ili kuona Ukristo wetu tunapotendewa na kutamkiwa mabaya tunabaki na msimamo ule wa kutorudisha ubaya kwa ubaya.”
Akiendelea na homilia yake, Askofu Mwasekaga aliwataka wanakwaya kuwa na fadhila ya utiii na unyenyekevu ili kudumisha mahusino mema kati yao na wale wanaowaongoza ili mipango na taratibu walizojiwekea ziweze kufikia malengo yake.
“Yesu alitii ndio maana akatukomboa, utii unaleta mafanikio, Mungu Baba alimtuma Mwana alitii.”
Kongomano hilio la UKWAKATA lilihusisha zaidi ya Wanakwaya 1500 kutoka Majimbo 32 Katoliki kati ya Majimbo 36 ambapo lilifunguliwa siku ya Ijumaa Septemba 12, 2025 kwa Adhimisho la Misa Takatifu iliyoadhimishwa na Mhashamu Wilbroad Henry Kibozi, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dodoma na kihitiimishwa Jumapili Septemba 14, 2025.